Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Ronald Makona amewataka Wakulima kuwa makini pindi wanapoenda kununua viuatilifu na kutoa onyo kwa Wafanyabiashara kuacha kuuza bidhaa bandia.
Ameyasema hayo wakati wa operesheni ya kukagua uwepo wa viuatilifu bandia, ambapo Taasisi ya Utafiti na Udhibiti wa Uiuatilifu (TPRI) imekamata kiuatilifu aina ya Dudu All 450 zaidi ya chupa 140 zenye ujazo wa lita moja na chupa 25 zenye ujazo wa nusu lita, katika duka linalouza pembejeo za kilimo la Asenga lililopo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Wakizungumzia operesheni ya kukagua uwepo wa viuatilifu bandia katika duka hilo, Mkaguzi Mkuu wa viuatilifu Kanda ya ziwa Richard Dastan, pamoja na Mkaguzi wa Afya ya mimea kutoka Holili Michael Shirima, wamesema uwepo wa viuatilifu bandia unawasabishia Wakulima kukosa mavuno na hivyo kushindwa kufikia malengo yao.
Kwa upande wake muuzaji wa pembejeo katika duka la Asenga, Paulo Mbega, amesema kitendo hicho ni funzo kwao, kwani haijawahi kutokea katika duka lao kuuza bidhaa bandia.