Aliyewahi kuwa Rais wa Marekani, Donald Trump amerudia madai yake kuwa ataweza kumaliza haraka vita kati ya Urusi na Ukraine kwa kuzungumza na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Katika mahojiano na Mtandao wa Right Side, Trump kwa mara nyingine amesema uvamizi wa Urusi usingetokea ikiwa bado angelikuwa ndani ya Ikulu ya White House.
Amesema, itawezekana kufanya mazungumzo ya kumalizika kwa vita ndani ya saa 24 kwani hiyo inawezekana ikiwa angekuwa kiongozi wa Marekani.
“Isingewahi kutokea, lakini ilifanyika lakini inaweza kujadiliwa, nadhani ndani ya saa 24 na hii ifanyike kutoka kwa ofisi ya rais na lazima uwapate wote wawili kwani kuna mambo ambayo unaweza kumwambia kila mmoja wao, ambayo sitayaweka wazi sasa.
Aidha, Trump amesema jumla ya vifo kutokana na mzozo huo ni kubwa kuliko kile kinachofichuliwa na kuongeza kuwa, “wanataja idadi ambazo hazilingani na uhalisia, wanapoangusha hizo nyumba kubwa za ghorofa, na kusema watu wawili wamekufa au watu watatu wameumia, si sawa.”
“Nadhani idadi ni kubwa zaidi na hiyo itafichuliwa baadaye, lakini tunapaswa kufanya kitu kuhusu hilo maana vita hivyo vinapaswa kukoma, na lazima vikome sasa, na ni rahisi kufanya hivyo,” ameongeza Trump.