Bingwa wa dunia wa masumbwi ya uzito wa juu, Tyson Fury usiku wa kuamkia leo amemchakaza kwa KO mpinzani wake Tom Schwarz katika pambano lililofanyika nchini Uingereza.
Fury alifanikiwa kumpiga bondia huyo Mjerumani katika raundi ya pili ya pambano hilo na kisha kupeleka ujumbe wa tambo kwa hasimu wake mkuu, Deontay Wilder ambaye walitoa sare katika pambano lao la kwanza.
Mwezi uliopita, Wilder pia alifanikiwa kushinda pambano lake kwa kumpiga Dominic Breazeale katika raundi ya kwanza.
Leo, Fury amewahakikishia mashabiki kuwa pambano la marudiano kati yake na Wilder litafanyika mwakani na kwamba anaamini atashinda tena kwa sababu hata wakimpiga chini hawawezi kumfanya abakie chini.
“Kulikuwa na farasi watatu kwenye uzito wa juu, sasa hivi tumebaki wawili, na huyo nilishampiga na nitampiga tena [mwakani],” alisema Fury.
“Labda hadi wakinipiga chini, wameshanipiga chini lakini hawakuweza kunifanya nibakie chini (KO), kwa namna hii bado nitaendelea kushinda,” aliongeza.
Mpiganaji huyo amemuondoa Anthony Joshua kwenye orodha ya wababe watatu kufuatia kipigo alichopokea hivi karibuni dhidi ya Andy Ruiz.
Kadhalika, amekumbuka jinsi alivyopigwa chini mara mbili na Wilder kwenye pambano lao la kwanza lakini hakubakia chini hadi raundi ya 12 na kutangazwa kuwa ilikuwa sare.