Shirika la mazingira la Umoja wa Ulaya – EEA, limesema kuwa uchafuzi wa hali ya hewa barani humo unaendelea kusababisha vifo 1,200 kwa mwaka huku wanaoathirika zaidi wakiwa ni watoto na wengine kuwa katika hatari ya kupatwa na magonjwa sugu.
EEA kupitia utafiti wake imesema, licha ya maboresho yaliyofanywa katika miaka ya hivi karibuni, kiwango cha vichafuzi muhimu vya hali ya hewa katika nchi nyingi za Ulaya bado kiko juu ya miongozo ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), haswa katika Ulaya ya Kati na Italia.
Utafiti huo uliofanyika katika zaidi ya nchi 30, ikiwa ni pamoja na zile 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya pia umebainisha kutoangazia hali ilivyo katika mataifa makubwa ya kiviwanda kama Urusi, Ukraine na Uingereza, jambo linaloashiria kuwa idadi ya vifo barani Ulaya kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa inaweza kuwa kubwa zaidi.
Novemba 2022, EEA ilitangaza kuwa Umoja wa Ulaya watu 238,000 walikufa mapema kwa sababu ya uchafuzi wa hali ya hewa sawa na mwaka 2020, idadi ambayo inajumuisha pia mataifa ya Iceland, Liechtenstein, Norway, Uswisi na Uturuki.