Rais wa Uganda, Yoweri Museveni ambaye pia ni mgombea urais katika uchaguzi mkuu nchini humo, ameeleza sababu za zilizopelekea serikali yake kuzuia mawasiliano yote ya simu, huduma za kibenki pamoja na mitandao ya kijamii leo ambapo wananchi wa nchi hiyo wamepiga kura.

Uamuzi wa Serikali kufunga mawasiliano ulikuja siku moja baada ya mpinzani wake Dk. Kiza Besigye kuwataka wananchi kuhakikisha wanalinda kura zao kwa kutumia simu zao kwa kupiga picha na kutoa taarifa popote ambapo wanaona kuna udanganyifu unafanyika.

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Kampala, Museveni ameeleza kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na Tume ya Mawasiliano nchini humo, ililenga katika kuzuia watu ambao wangeweza kuhatarisha usalama.

“Hizi ni hatua za kiusalama za kuzuia watu wengi kuzua vurugu. Ni hatua ya muda tu. Itaondolewa. Ni kwa sababu watu wengi hutumia vibaya njia hizi, kueneza uongo. Iwapo unataka kujivunia haki fulani, basi itumie vyema,” alisema Museveni.

Idadi kubwa ya wananchi wa Uganda wamejitokeza kupiga kura, hali iliyopelekea Tume ya Uchaguzi kuongeza muda wa saa moja katika baadhi ya maeneo ambayo yalionekana kuwa na idadi kubwa zaidi ya wapiga kura.

Zoezi la kupiga kura limekamilika na tayari kura zilianza kuhesabiwa tangu majira ya saa kumi na moja.

Yoweri Museveni anachuana vikali na Dk. Kiza Besigye na Amama Mbabazi.

Ajabu: Mfungwa ajidunga 'mimba' kukwepa adhabu ya kunyongwa
Ronaldo Afichua Siri Nzito Iliyodumu Kwa Miaka Minane