Scolastica Msewa, Kibaha – Pwani.

Meneja wa kituo cha Uhakiki wa Vipimo Misugusugu, Charles Mavunde amesema uhakiki wa matanki ya Malori ya kubebea vimiminika husaidia kurahisisha ukadiriaji wa bei za bidhaa na upatikanaji wa huduma kwa Wananchi hivyo amewataka wenye malori hayo watoe ushirikiano wa kuhakiki ujazo wa matanki yao kila mwaka.

Akizungumza na Wandishi wa Habari, Mavunde amesema iwapo muuzaji atauza kwa kipimo sahihi bila kupunja na mnunuzi akanunua kwa kipimo sahihi bila kupunjwa hupelekea anayepanga bei kwa mlaji wa mwisho kupata nishati kwa bei rahisi.

“Nitoe wito kwa bohari za mafuta, gesi na mafuta ya kula kuhakikisha kwamba wamezingatia Sheria ya Vipimo Sura 340 ili kila mteja anayehudumiwa tenki lake liwe limehakikiwa na Wakala wa Vipimo lina chati ya mwaka husika,” amesema Mavunde.

Aidha, ameongeza kuwa, “kabla ya kutumia wahakikishe kwamba bohari za vimiminika hivyo, wauzaji wa nishati hizo na watumiaji mmoja mmoja wahakikishe yamehakikiwa katika kituo chetu au katika vituo vya mikoa.”

Alisema kituo cha uhakiki wa Vipimo Misugusugu Kibaha, huhakiki matenki yabebayo vimiminika wastani wa 500 uwezo wake ni kuhakiki malori 70 kwa siku ikiwa ni maboresho ya kutoka Wakala hao kupima malori 8 kwa siku Ilala jijini Dar es salaam kwa lengo la kuhakikishia vipimo sahihi kati ya mbebaji na mnunuzi wa kimiminika.

Alisema kwa sasa wastani wa malori 30 huhakikiwa kwa siku katika kituo hicho ingawa kituo hicho cha Misugusugu kina uwezo mkubwa kuhakiki malori hadi 70 kwa siku ikiwa idadi hiyo hupungua kutokana na uwepo wa vituo vya uhakiki huo katika mikoa ya Iringa, Mwanza, mtwara na Arusha.

Amesema Wakala wa Vipimo wapo tayari kufanya kazi na wauzaji na wasambazaji wa mafuta na gesi ili biashara zao ziwe na tija kwao, kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa Taifa zima, ili kuimarisha uchumi wa Taifa.

Idadi ya Waliofariki ajali ya Hiace Kagera yaongezeka
Baleke, Chama, Saido kuongezewa dozi Simba SC