Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa mzani katika bandari ya Kemondo uliogharimu kiasi Cha Shilingi milioni 34 mkoani Kagera ni miongoni mwa mwendelezo wa njia zinazotumika kupata idadi  halisi ya mzigo unaoingia na kutoka bandarini hapo ili kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato. 

Ameyasema hayo mkoani Kagera, wakati akifungua rasmi mzani huo, amesema Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kukusanya mapato hivyo itaendelea kuwekeza fedha kwenye miudombinu ili kuziimarisha kimapato na kuongeza tija. 

“Kumekuwa na mianya mingi ya upotevu wa mapato katika maeneo mbalimbali hivyo tunaimarisha miuondombinu sambamba na mifumo hivyo nina Imani uwepo wa mzani huu tutajua sasa mzigo unaoingia na kutoka na kudhibiti mapato”, Amesema Naibu Waziri Mwakibete. 

Aidha ameitaka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuharakisha taratibu za manunuzi kwa ajili ya mradi upanuzi wa bandari ya Bukoba, Kemondo na Mwanza ili kwenda sambamba na ukamilikaji wa meli ya MV Mwanza. 

Naye Kaimu Menenja wa Bandari za Ziwa Viktoria, Vicent Stephen, amesema maboresho yaliyofanywa kwa bandari ya Kemondo yameongeza huduma ya shehena kufikia tani 9,652 kwa mwaka 2022 ikilinganisha na tani 3,436 kwa mwaka 2021 na kupandisha mapato kufikia milioni 165 kwa mwaka 2022 kulinganisha na 108 kwa mwaka 2021. 

Stephen ameongeza kuwa kwa mwaka 2021/22 Mamlaka imetenga bilioni 8 kwa ajili ya kuboresha gati, jengo la abiria, uzio na miuondombinu mingine katika bandari ya Kemondo ili kuruhusu meli ya MV Mwanza kapakia na kupakua mizigo itakapoanza huduma. 

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi-Uchukuzi, Atupele Mwakibete yuko mkoani Kagera kwa ziara ya siku mbili kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya sekta inayoendelea mkoani humo.

TBS yatoa elimu kwa wahariri
Uingereza yalizishwa na utendaji kazi wa Tanzania