Wabunge wa Ukawa wameelezea sababu zilizowafanya kuchukua uamuzi wa kupiga kelele baada ya Rais wa Zanzibar, Dkt Ali Mohamed Shein kuingia Bungeni hali iliyopelekea kutolewa nje ya Bunge hilo.

Mbunge wa jimbo la Hai ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, Freeman Mbowe alieleza kuwa walishindwa kuvumilia kuona ujio wa Dkt Shein akiingia Bungeni hapo pamoja na msheshimiwa Pandu Kificho ambaye alidai hivi sasa sio Spika wa Baraza la Wawakilishi kwa kuwa Baraza hilo lilikwisha vunjwa.

“Tumeshangaa kuona Pandu Kificho anaingia kama Spika wa Baraza la Wawakilishi wakati Baraza limeshavunjwa, tulishangaa kuona Dkt Shein anaingia kama Rais wa Zanzibar wakati huo kipindi chake cha kukaa madarakani miaka mitano kimekwisha kikatiba,” alisema Mbowe.

Naye mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alisisitiza kuwa wataendelea kuonesha msimamo wao huku akimlalamikia Spika wa Bunge hilo kuwa anaendesha Bunge kibabe.

“Leo hii askari wenye uniform, mae-FFU… askari wa fujo wameingia ndani ya ukumbi wa Bunge. Sasa kwa wasiofahamu, ukumbi wa Bunge katika nchi kama za kwetu na nchi zinazofuata utaratibu kama wa kwetu, ukumbi wa Bunge huwa haingii mtu yoyote asiyekuwa Mbunge. Ndio maana ili Makamo wa rais na wale wakubwawakubwa tuliokuwa tunawapigia kelele… waingie, ilibidi tutengue kanuni ili kuwaruhusu waingie,” alisema Tundu Lissu.

Mwenyekiti wa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Juma Hamad Omary alimtaja Maalim Seif Sharif Hamad kuwa kiongozi anayepaswa kuigwa kwa kuwa aliwahi kukubali kushindwa mara kadhaa licha ya mapungufu kuonekana na kwamba hata alipokuwa Makamu wa Kwanza wa rais na kisha wawakilishi wa CCM kukataa asuhudhurie kwenye sherehe za kufunga Baraza la Wawakilishi, aliamua kutohudhuria.

TACCEO watoa ripoti ya Uchaguzi Zanzibar, waeleza kuwepo unyanyasaji wa Kijinsia, Waishauri ZEC
Jumba La Milioni 500 Lakumbwa Na Bomoabomoa Dar, Mmiliki Alia Na Kesi