Operesheni ya kubomoa nyumba zilizojengwa kinyume cha sheria katika maeneo ya wazi inayoendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imedhihirisha kutowalenga watu wa maisha ya chini pekee baada ya kuanza kuwagusa watu wenye ‘ukwasi’.

Jumba la ghorofa moja lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500 lililoko katika eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam jana lilikubwa na operesheni hiyo na kubomolewa huku mmiliki wa jengo hilo, Bi. Catherine Kisiliwe akipewa muda wa dakika 30 hadi 40 kuhakikisha anaokoa mali zake zote.

“Sisi hatukuja hapa kuchukua maelezo, sisi tumekuja hapa kutekeleza maagizo na sheria,” Mhandisi wa Wilaya ya Kinondoni, Baraka Mkuya alimwambia Bi. Catherine aliyejaribu kutoa utetezi wake kuwa kesi hiyo iko mahakani na kudai kuwa vielelezo vya kesi hiyo anavifuata mumewe.

Hata hivyo, Bi. Catherine ambaye alionekana kulia na uwepo wa kesi inayoendelea mahakamani alishindwa kutoa vitu vyake kwa kushikwa na butwaa. Lakini vijana waliokuwa katika eneo hilo waliingia ndani ya jumba hilo na kumsaidia kuokoa mali zake ikiwa ni pamoja na magari yake.

Akizungumzia tukio hilo, Mhandisi Mkuya alisema kuwa kuna tabia imejengeka ya watu wenye kipato cha juu kuvamia maeneo ya wazi na kujenga au kuwanyang’anya watu wa kipato cha chini viwanja na kujenga majumba ya kifahari. Alisema operesheni hiyo itafuata sheria bila kujali kipato cha mtu yeyote.

Zaidi ya nyumba 20 zilibomolewa jana katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam.

 

Ukawa waeleza sababu za kuzomea Bungeni Na Watakachofanya Baadae
Magufuli Aagiza Mamilioni Ya Kumpongeza Yakanunue Vitanda Muhimbili