Ikiwa hii leo ni siku ya kimataifa ya makazi duniani, Umoja wa Mataifa (UN), unataka hatua zichukuliwe kuhakikisha ukuaji wa miji unakuwa jumuishi kwa watu wote na kuhakikisha huduma muhimu za kijamii zinapatikana.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii yenye maudhui ya ‘Zingatia pengo lililoko, usimwache nyuma mtu yeyote au eneo lolote, anasema ukuaji wa miji lazima uende sambamba na uwekezaji ikiwemo uwezo wa watu kupata nyumba za kuishi.
Amesema, ujumbe huo unatambua ongezeko la pengo la ukosefu wa usawa katika mazingira ya kuishi duniani kote, na kwamba mlolongo wa changamoto, kuanzia majanga ya tabianchi, vita na Uviko-19, kuathiri watu wengi Duniani, na kwamba kasi kubwa ya ukuaji wa miji inachochea changamoto hizo na zaidi ya watu bilioni moja wanaishi kwenye makazi duni.
Hata hivyo amesema, hatua na uwekezaji zaidi zinahitajika kwenye makazi ambayo watu wanaweza kumudu, sambamba na huduma za nishati ya umeme, maji, huduma za kujisafi, usafiri na nyingine za msingi.