Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi Hyera amewataka Wafanyabiashara kutoa ushirikiano kwenye suala la ulinzi, jambo ambalo litasaidia kuepusha vitendo vya uhalifu kwenye maeneo yao.
Hyera ameyasema hayo wakati alipokutana na wafanyabiashara wa Soko Kuu la Ichenjezya la Wilayani Mbozi na kudai kuwa suala la kuimarisha ulinzi haliepukiki na kuwataka kulitilia mkazo, ili kuudhibiti uhalifu.
Lengo la kufika Sokoni hapo lilikuwa ni kuzungumza na Wafanyabiashara ili kuwaelimisha kuhusu masuala mbalimbali ya kudhibiti uhalifu na wahalifu, ukiwemo ule unaotendeka kwa njia ya mtandao.
Koplo wa Polisi, Magere ambaye ni mtaalamu katika eneo la kupambana na makosa ya uhalifu kwa njia ya mtandao aliwataka wafanyabiashara hao kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuepuka kutapeliwa kupitia ujumbe wa simu ya mkononi na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu matapeli, ili hatua zichukuliwe.
Kwa upande wao Wafanyabiashara wa soko hilo wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa hatua wanazoendelea kuzichukua, sambamba na kuwaelimisha Wananchi kuhusiana na masuala mbalimbali ya kiusalama.