Serikali, imevunja Kamati ya Mipango Miji ya Jiji la Mwanza iliyokuwa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi na Mipango miji wa Jiji hilo, Hamidu Said na Katibu wa Kamati ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Yahya Sekieti.
Hatua hiyo imechukuliwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula hii leo, wakati wa kikao kazi cha viongozi wa sekta ya ardhi ngazi ya wilaya, mitaa, kata na Mkoa kwa madai ya uwepo wa dhuluma katika ardhi.
Amesema, “tunaenda kuchukua maamuzi magumu kwa ushauri pamoja na Waziri wa Tamisemi, Kamati ya Mipango Miji ya Jiji la Mwanza inaenda kuvunjwa na hakuna mjumbe hata mmoja atakaetakiwa kurudi tena kwenye kamati ile.”
Aidha, Dkt Mabula ameongeza kuwa, Mkoa wa Mwanza umekuwa na sifa ya kudhulumu ardhi za wazee na wajane na kwamba suala la utoaji wa vibali vya ukarabati wa majengo nalo limekuwa likiendeshwa kinyume.
Amezitaka halamshauri zote nchini kutenga maeneo ya uwekezaji na kuyalinda kwa ajili ya kupokea wawekezaji, na kuagiza viongozi wa kuanzia ngazi ya mtaa, kata tarafa, wilaya mpaka mkoa kwa kila mwenye dhamana kutatua migogoro ya ardhi.