Urusi imetoa kauli yake kuhusu maandalizi ya mkutano wa kihistoria yanayoendelea kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un.
Akizungumza hivi karibuni, Rais wan chi hiyo, Vladimir Putin amesema kuwa nchi yake itahakikisha kuwa mkutano huo unafanikiwa huku akitoa tahadhari ya ziada.
Rais Putin amezitaka nchi za Magharibi pamoja Urusi yenyewe kuihakikishia Korea Kaskazini usalama na maendeleo ya kiuchumi ili mkutano huo uzae matunda ya kudumu.
“Tutakuwa tunasubiri matokeo ya mkutano kati ya Rais Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un na tutatoa ushirikiano kufanikisha mkutano huu kadiri iwezekanavyo,” alisema Rais Trump.
Aidha, alizitaka nchi zote kuipa ushirikiano Korea Kaskazini endapo mkutano huo utafanikiwa na nchi hiyo kuachana na mpango wake wa silaha za kinyuklia.
Hivi karibuni, Rais Trump alisema kuwa Korea Kaskazini inaweza kuwa nchi tajiri baada ya kuachana na mpango wake wa kinyuklia na kufunguliwa mlango wa kuungana na dunia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alisistiza kuwa Trump anapaswa kumhakikishia ulinzi Kim Jong Un ili kufanikisha mpango wao.
Trump na Kim wanatarajiwa kukutana Juni 12 mwaka huu nchini Singapore kuandika historia ya kwanza ya viongozi wa juu wa nchi hizo mbili walioko madarakani kukutana kwa mara ya kwanza.