Licha ya Serikali ya Ukraine kuweka shinikino kwa Wanachama, Urusi imechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa urais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, lenye Wajumbe wa kudumu wa nchi za Uingereza, Marekani, Ufaransa na China.
Baraza la wajumbe 15, huchukua nafasi ya urais kwa mwezi mmoja kwa utaratibu wa kupokezana ambapo mara ya mwisho Urusi kuwa na nafasi ya urais ni Februari 2022, mwaka ambao ilianzisha uvamizi kwa Ukraine.
Hatua hiyo, inafanya Baraza la Usalama kuongozwa na nchi ambayo rais wake yuko chini ya hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa madai ya uhalifu wa kivita wa kulivamia na kulishambilia Taifa la Ukraine.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu – ICC, ambayo si taasisi ya Umoja wa Mataifa ilitoa hati ya kukamatwa kwa Rais Vladimir Putin mwezi Machi na licha ya malalamiko ya Ukraine, Marekani ilisema haiwezi kuizuia Urusi kutwaa kiti cha urais.