Matokeo ya utafiti uliofanywa na jopo la madaktari bingwa wa Harvard Medical School umebaini kuwa uongozi wa kisiasa wa nchi hupunguza umri wa kuishi na kwamba ni hatari kwa afya ya mhusika.

Utafiti huo uliowahusisha viongozi 279 wa mataifa 17 ulibainisha kuwa msongo wa mawazo pamoja na shinikizo ni chanzo kikuu cha kupunguza umri wa kuishi wa viongozi hao kutokana na kudhoofisha afya zao.

Hii inatokana na matatizo mengi yanayozikabili nchi mbalimbali huku wananchi wakielekeza matumaini yao yote kwa viongozi hao kuyatatua.

Jopo la watafiti hao walitumia njia ya kufuatilia umri wa kufariki wa viongozi walioingia madarakani na kulinganisha na umri wa kufariki wa wapinzani wao ambao hawakufanikiwa kuingia madarakani kuwatumikia wananchi.

Kufuatia njia hiyo, walibaini kuwa muda wa kuishi wa viongozi waliokuwa madarakani ulishuka kwa miaka mitatu ukilinganisha na wapinzani wao.

Akitoa mfano wa mahojiano waliyofanya na baadhi ya viongozi wastaafu wa mataifa mbalimbali, kiongozi wa utafiti huo, Dk. Anupam Jena alieleza kuwa majukumu yaliwafanya viongozi hao kushindwa kula vizuri na kufanya mazoezi.

Alieleza kuwa rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton alilieleza jopo hilo kuwa huenda aliishia kula vyakula visivyofaa kutokana na kuwa na msongo wa mawazo na mfadhaiko.

“Labda, kama ulimwengu ungelikuwa na amali, mtindo wa maisha ya viongozi ungelikuwa tofauti,”alisema Dk. Jena.

Chanzo :BBC

Mkutano Mkuu Wa TFF Waahirishwa
Julio Ampongeza Rais Magufuli Kuhusu Nape