Rais John Magufuli ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kurekebisha dosari zilizopo katika mfumo wa utoaji mikopo ya elimu ya juu ili kuepuka usumbufu uliojitokeza kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza.

Akizungumza leo alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa hosteli za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Magufuli ametaja dosari zilizopo katika utoaji wa mikopo hiyo kuwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa upendeleo, kutozingatia sifa stahiki za wanafunzi, mikopo hewa na ucheleweshwaji wa mikopo.

Aidha, Rais Magufuli aliagiza Wizara ya Elimu, Wizara ya Fedha, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu pamoja na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wenye sifa ya kupata mikopo wanapata mikopo hiyo kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kujipanga kukusanya marejesho ya mikopo kwa wote waliokopeshwa na bodi hiyo ambapo mpaka sasa Bodi hiyo inada takribani shilingi trilioni 2.6.

Rais pia aliwataka wanafunzi hao kuzingatia masomo na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa sheria na taratibu wakati Serikali inaendelea kurekebisha dosari zilizopo.

Naye Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako aliwahakikishia wanafunzi kuwa changamoto ya mikopo yao itatatuliwa ipasavyo na kwamba tayari Wizara hiyo imeshatoa mikopo kwa idadi kubwa ya wanafunzi.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alipongeza Wakala wa Majengo Tanzania, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa hatua kubwa ya ujenzi iliyofikia tangu uanze Julai Mosi mwaka huu.

Video: Mfalme wa Morocco kutua Dar na ndege sita kubwa
Video: Mfalme wa Morroco kutua Dar na ndege sita kubwa