Waziri wa Nchi, Ofisi Rais (TAMISEMI), George Simbachawene ameagizwa kuhakikishe Halmashauri zote zinakamilisha ujenzi wa maabara za sayansi ili vifaa vilivyoletwa visikae bohari kwa muda mrefu.

Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa leo Juni 6, 2017 wakati akizungumza na viongozi, walimu na wanafunzi wa shule za sekondari wanaosoma masomo ya sayansi waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa usambazji wa vifaa vya maabara kwa shule za sekondari Tanzania bara iliyofanyika kwenye viwanja vya Lugalo jeshini, jijini Dar es salaam.

“Vifaa vya maabara vitatolewa katika shule za Tanzania Bara zilizokamilisha majengo na miundombinu muhimu ya maabara. Hivyo, ni vizuri sasa Halmashauri zote ambazo shule zake hazijakamilisha ujenzi wa maabara ziongeze bidii ili ziweze kunufaika na utaratibu huu. Mheshimiwa Waziri wa Nchi TAMISEMI simamia suala hili,” amesema.

Pia, Waziri Mkuu amemwagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako ahakikishe anawasiliana na Waziri mwenzake wa Zanzibar ili wabadilishane uzoefu na utaratibu huo uweze kuzinufaisha pande mbili za Muungano.

“Tunapoimarisha elimu nchini ni vizuri jitihada hizi zikahusisha pande zote mbili za Muungano. Hivyo, wekeni utaratibu wa kubadilishana uzoefu na wenzetu wa Zanzibar, ili jitihada hizi zinufaishe pande zote mbili za Muungano,” amesema.

Video: IGP Sirro afanya ziara Kibiti, Rufiji, atangaza msako mkali
Video: Anna Mghwira aahidi kutomwangusha JPM