Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) imechangia kwa kiasi kikubwa katika kuhakikisha kuwa upatikanaji wa maji safi na salama nchini unaongezeka.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda wakati akizungumza na waandishi wa habari, amesema kuwa katika kuadhimisha Wiki ya Maji, Mkoa wa Dar es Salaam umelenga kuwahamasisha na kuwa elimisha Wananchi, Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na Kamati za Maji kuhusu namna bora ya usimamizi wa shughuli za maji katika maeneo yao ikiwemo na taratibu za umiliki wa visima.

Amesema kuwa, lengo la maadhimisho hayo ni kuongeza upatikanaji wa maji, uzalishaji na usambazaji wa maji safi na salama ambayo yatatumika kwa uangalifu ili kupunguza kiwango cha matumizi yake.

Ameongeza kuwa, hali ilivyo sasa, kiwango kikubwa cha Majitaka kutoka viwandani na majumbani kinaachwa kutiririka bila kutibiwa na kurudishwa kutumika tena ambapo jambo hilo husababisha virutubisho vingi vilivyomo katika maji hayo kupotea.

“Katika kuhakikisha maendeleo endelevu na mzunguko wa uchumi, Majitaka ni rasilimali muhimu na hivyo kuyasindika, kuyasafisha kwa kuyatibu na kuyatumia tena ni jambo la lazima”, Amesema Makonda.

Aidha, ameongeza kuwa, katika maadhimisho ya Wiki ya Maji, shughuli za usafi na upandaji miti katika maeneo ya vyanzo vya maji zitafanyika, miradi mitatu ya maji katika maeneo ya Mbagala pamoja na Pugu itazinduliwa na pia miradi 20 ya Jamii itakabidhiwa rasmi DAWASCO.

Hata hivyo, Makondaa ameongeza kuwa, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wakazi wa Dar es Salaam ni asilimia 75 ambapo uzalishaji wa maji hayo kwa sasa ni lita Milioni 390 kwa siku wakati mahitaji ya maji hayo kwa sasa ni ni lita Milioni 510 kwa siku.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) Kiula Kingu amesema kuwa, DAWASCO pamoja na DAWASA wamefanikiwa kuzuia upotevu wa maji kwa kiasi kikubwa ambapo kwa mwaka jana ulikuwa  ni asilimia 47 na mwaka huu umepungua na kufikia asilimia 38.6.

Naye Meneja Mahusiano ya Jamii Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASA) Neli Msuya amesema kuwa, maeneo yote ya Dar es Salaam yasiyo na mtandao wa maji yamekuwa yakitengenezewa ramani (design) ili yawekewe mitandao hiyo ya maji ili maji yaweze kupatikanakwa wakazi wa maeneo hayo.

 

Jinsi familia zinavyoathiriwa na teknolojia
Mzimu Wa Lukaku Kumuandama Ronald Koeman?