Aliyekua mchezaji wa klabu ya Chelsea Ray Wilkins amemtaka meneja wa klabu ya Everton Ronald Koeman kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, endapo uongozi utashindwa kumbembeleza Romelu Lukaku ili akubali kubaki Goodison Park.

Lukaku tayari ameshaueleza uongozi wa klabu hiyo, hatosaini mkataba mpya, kutokana na hitaji la kutaka kusaka changamoto mpya ya soka lake.

Wilkins ametoa ushauri huo alipohojiwa na talkSPORT, kwa kuhofia huenda meneja huyo kutoka nchini Uholanzi akakosa muelekeo wa kukiongoza kikosi cha Everton, ambacho kwa sasa kinategemea uwezo wa Lukaku katika harakati za kusaka ushindi.

Wilkins ambaye pia aliwahi kukinoa kikosi cha Chelsea kwa muda, amesisitiza kuwa, kuondoka kwa Lukaku huenda kukavunja umoja na mshikamano ambao kwa sasa unaonekana miongoni mwa wachezaji wa klabu hiyo.

“Ni hakika kwa sasa Everton ina umoja na mshikamano, na kama itatokea mmoja wa wachezaji anaondoka katika kipindi hiki ambacho Koeman ameshaweka mguu sawa kwenye ushindani wa michezo ya ligi, kuna hatari ya mipango hiyo kuvurugika.

“Ninahofia kuporomoka kwa Everton na kurudi ipokua, klabu hii ilikua inaonekana ya kawaida dhidi ya timu pinzani za ligi kuu, hivyo kuna ulazima kwa Koeman kufikiria mara mbili kuhusu mchakato wa kuondoka kwa nguvu kazi yake ambayo ni Lukaku.

“Viongozi wanapaswa kufanya kazi ya ziada ya kukaa chini na Lukaku, ili kumjengea mazingira ambayo yatamzuia kuondoka klabuni hapo, na hata ikitokea anaondoka, bado watatakiwa kusuka mpango wa kumsajili mchezaji mwenye kiwango cha juu ili kuziba pengo lake.

“Kama itatokea uongozi unashindwa kufanya mambo hayo mawili, hofu yangu itaendelea, na sitochoka kumuomba Koeman aondoke ili akatafute changamoto mpya ya ukufunzi mahala pengine.” Alisema Willkins.

Video: Makonda aipongeza Dawasco kwa kutoa huduma nzuri za maji
Samia Suluhu amwakilisha Rais Magufuli mkutano wa wakuu wa nchi