Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kumteua kuwa mkuu wa mkoa huo.
Makonda metoa shukrani hizo mapema hii leo wakati wa hafla iliyofanyika Osterbay Jijini Dar es salaam ya kutimiza mwaka mmoja katika Mkoa wake wa Dar es salaam, amesema kuwa amepitia katika maisha magumu mpaka kupata nafasi hiyo ya kuongoza Mkoa Mkubwa kama Dar es salaam.
Aidha, pamoja na hayo Makonda amewashukuru viongozi mbalimbali wa Serikali kwa ushirikiano wanaompatia kwani Serikali ya awamu ya tano inafanyakazi kwa umoja na ushirikiano.
Hata hivyo, amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuwawezesha wananchi kujikwamua na kuondokana na wimbi kubwa la vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya.
Makonda amesema kuwa mkoa wa Dar es salaam umeendelea kuwa na hali nzuri ya usalama na amani kwani umepunguza idadi kubwa ya matukio yaliyokuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Pia ametoa onyo kwa wakandarasi wote wanaojenga barabara chini ya kiwango vinginevyo watarudia barabara hizo kwa gharama zao.
Vile vile amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano inapambana na watu ambao wanaharibu ndoto za wananchi na kuwarejesha kwenye ndoto zao.