Mhamiaji kutoka Mali amepewa sifa na kutunukiwa uraia wa Ufaransa baada ya kufanya tendo la kishujaa kwa kumuokoa mtoto mdogo aliyekuwa ananing’inia kwenye kibaraza cha ghorofa ya nne katika jengo refu jijini Paris.
Mamoudou Gassama, mwenye umri wa miaka 22 alipanda jengo hilo refu bila kutumia vifaa vyovyote huku akishangiliwa na watu waliokuwa wamekusanyika nje ya jengo hilo, hadi kufanikisha kumfikia mtoto huyo wa kiume mwenye umri wa miaka minne.
Kitendo hicho cha kishujaa kilichofananishwa na ushujaa uliwahi kuoneshwa na ‘Spiderman’, uliteka mitandao ya kijamii huku video yake ikivuta hisia za wengi waliotaka atunukiwe uraia na maisha bora kwa kujitoa kuokoa maisha.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron alimualika kijana huyo Ikulu na kuzungumza naye, kisha akampa cheti maalum cha kutambua ushujaa wake na kuamuru apewe uraia wa Ufaransa baada ya kusikia jinsi alivyohangaika kuingia nchini humo.
Rais Macron pia alimtunukia medali ya kipekee ya ushujaa kijana huyo na kuwataka raia wote kuiga mfano wake.
Katika mazungumzo yake na Rais Macron, Gassama ambaye aliingia nchini Ufaransa kwa mahangaiko akitumia usafiri wa boti ndogo kutoka nchini Mali kupitia bahari ya Mediterranean na nchini Italia, alisema kuwa aliwaona watu wakiwa wamezunguka eneo la jengo hilo wakimshangaa mtoto aliyekuwa analia juu ya jengo akihitaji msaada na ndipo alisikia amepata ujasiri wa kupanda jengo hilo kwa mikono mitupu.
Tukio hilo lililobadili maisha ya kijana huyo wa Ghana lilitokea Jumamosi jioni katika mitaa ya kaskazini mwa jiji la Paris.
“Nilipowaona watu wamezunguka wanashangaa, sikuwa na muda wa kufikiria, nilikimbia nikavuka barabara kwenda kumuokoa mtoto,” alimwambia Rais Macron.
“Nilipanda jengo, namshukuru Mungu, Mungu alinisaidia. Kadiri nilivyozidi kupanda nilipata ujasiri wa kupanda zaidi, ilikuwa hivyo,” aliongeza.
Alisema kuwa alipomfikia mtoto alibaini kuwa tayari mtoto alikuwa na jeraha kwenye mguu wake.
Kikosi cha zima moto na uokoaji kilipowasili kilibaini kuwa tayari mtoto alikuwa ameshaokolewa na msamalia mwema na Mkurugenzi wa kikosi hicho hakusita kutoa pongezi zake kwa muokoaji.
Baba wa mtoto huyo anashikiliwa na anahojiwa na jeshi la polisi kwa kosa la kumuacha mtoto mdogo nyumbani bila muangalizi. Mama wa mtoto huyo ameripotiwa kuwa hakuwa jijini humo.