‘Tanzania got talent’, ndicho anachokiamini hivi sasa Rais wa Marekani, Donald Trump baada ya kuiona video ya mwanamke Mtanzania, Hadhara Charles Mjeje (29) akipiga danadana hata zaidi ya baadhi ya wachezaji wa Ligi kubwa za kulipwa duniani.
Trump, kama ilivyo kwa watu wengine aliiona video hiyo kupitia mtandao wa Twitter, ikiwa imewekwa Februari 19 mwaka huu na mtu mmoja anayetumia jina la Akin Sawyerr. Mtumiaji huyo aliandika kwenye post ya video hiyo, “talents are evenly distributed, opportunity isn’t”. Kwa tafsiri isiyo rasmi ya Kiswahili, “vipaji vinagawanywa kwa usawa, fursa hazina mgawanyo sawa.”
Rais huyo wa taifa lenye nguvu duniani na mtumiaji mkubwa wa mtandao wa Twitter, ali-retweet na kuandika, “Amazing!” Yaani “Inashangaza!”
Amazing! https://t.co/uUNCL1hPAk
— Donald J. Trump (@realDonaldTrump) February 19, 2019
Tweet hiyo hadi sasa imepata Likes 122,000, na Retweet zaidi ya 33,966. Hivyo, kuipa umaarufu zaidi. Imepata nafasi ya kuandikiwa habari kwenye vyombo vikubwa duniani; wengi wamemtafuta Hadhara Charles Mjeje na kumhoji.
Hata hivyo, sio wote waliopenda namna ambavyo Trump alipagawa na video hiyo, hususan wale wakosoaji wake wanaopinga karibu kila kitu anachofanya. Baadhi ya Wamarekani walimkosoa wakidai kuwa wasingetegemea kumuona Rais wao anapagawa na video hiyo wakati nchi iko kwenye kipindi cha dharura kwa siku tatu.
Mbali na Rais Trump, video hiyo ambayo imeshatazamwa zaidi ya mara milioni 9 kwenye YouTube, imewavuta watu wengine wakubwa duniani akiwemo mtangazaji maarufu wa Uingereza, Piers Morgan ambaye ameipost na kuandika, “BRILLIANT”.
Kwa mujibu wa mahojiano aliyofanya na mtandao wa Ruptly wa Urusi, mwanamke huyo ameeleza kuwa video hiyo ilichukuliwa Lilongwe nchini Malawi, Januari mwaka huu, alipoenda kwa ajili ya kufanya maonesho na kujikusanyia fedha.
Hadhara ameeleza kuwa anazunguka nchi kadhaa barani Afrika kwa lengo la kutafuta fedha kupitia kipaji chake, kwa ajili ya kuihudumia familia yake, kwani ni mama wa watoto wawili wa kiume.
Amesema kuwa alianza kupiga danadana tangu akiwa na umri mdogo, lakini alifanya mazoezi zaidi kwa kipindi cha miaka sita mfululizo, na sasa uwezo wake umekuwa mara elfu kadhaa kiasi kwamba wengi wanadhani anatumia uchawi.
“Wengine wanadhani ninatumia uchawi, lakini sio kweli. Hakuna kitu chochote ndani ya huu mpira. Ninatumia kipaji ambacho nimeanza kukitengeneza miaka sita iliyopita. Ni kipaji halisi, sio uchawi,” amesema hadhara.
“Ninawapenda wachezaji wa soka kama Messi, Cristiano Ronaldo na Ronaldinho,” ameongeza.
Mtandao wa RT wa Urusi umeandika kuwa, hivi sasa kwa uwezo wake amekuwa mshindani wa wachezaji hao wakubwa waliowataja linapokuja suala la uwezo wa kupiga danadana.
“Mimi ninapiga danadana ya kichwa mara 5,800 nikiwa nimeketi chini,” alisema Hadhara. Je, Messi, Ronaldo, Ronaldinho hii wanaweza hilo?
Amesema hadi sasa ameshatembelea nchi za Afrika Kusini, Gabon, Cameroon, Ethiopia, Kenya, Mawili na Msumbiji na analipwa wastani wa kiasi cha Tsh. 10,000 ($4) kwa kuonesha danadana kwa dakika mbili.