Mapambano yaliyopatikana katika muongo mmoja uliopita dhidi ya vifo vya uzazi na watoto wachanga yanatabiriwa kupungua barani Afrika na hivyo kuweza kuleta athari za moja kwa moja kwa wajawazito na watoto.
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, imesema ramani ya takwimu za afya Afrika kwa mwaka 2022 imetathmini maeneo tisa yanazohusiana na lengo la 3 maendeleo endelevu (SDG) kuhusu afya.
Ramani hiyo imegundua kuwa, kwa kasi ya sasa unahitajika uwekezaji zaidi ili kuharakisha maendeleo na kufikia malengo hayo magumu huku ikikadiriwa kuwa wanawake 390 watakufa wakati wa kujifungua kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Idadi hiyo, ni zaidi ya mara tano zaidi ya lengo la ajenda ya mwaka 2030 la vifo vya chini ya 70 vya uzazi kwa kila vizazi hai 100 000, huku ikiwa juu kuliko wastani wa vifo 13 kwa kila watoto 100 000 wanaozaliwa hai iliyoshuhudiwa barani Ulaya mwaka 2017 na pia ni zaidi ya kiwango cha kimataifa cha wastani wa vifo 2011.