Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuchunguza matumizi ya Tsh. Bilioni 15.3 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia matumizi ya Mamlaka ya Usafiri wa Reli Tanzania na Zambia (TAZARA)

Ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA jijini Dar es salaam muda mfupi mara baada ya kuwasili kwa Treni akitokea Fuga Rufiji mkoani Pwani ambako aliweka jiwe la msingi katika mradi wa kuzalisha umeme wa mto Rufiji.

Fedha hizo zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ukarabati wa injini 7 ambazo zingewezesha kusafirisha tani laki 4 za mizigo na kugharamia ununuzi wa mitambo ya mgodi wa kokoto za ujenzi wa reli na kuboresha miundombinu ya reli katika stesheni ya fuga.

Aidha, pamoja na kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli amewahakikishia wafanyakazi wa TAZARA kuwa serikali haiwezi kuicha TAZARA ife hivyo atazungumza na Rais wa Zambia, Edgar Lungu ili wachukue hatua madhubuti za kununua Injini na Mabehewa.

”Nimesafiri na Treni ya Tazara, nimejionea mwenyewe, niwahakikishie kwamba nitaelekeza nguvu zangu Tazara,”amesema Rais Magufuli

Kwasasa TAZARA ambayo reli yake ina uwezo wa kusafirisha tani milioni 5 kwa mwaka inahitaji injini 15 za Treni ya mizigo, Injini 4 za Treni ya abiria na mabehewa 700 ili angalau iweze kusafirisha tani laki 6 za mizigo kwa mwaka zitakazo zalisha faida.

 

Kuiba ni dhambi, mkiiba mnajiibia wenyewe- JPM
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 27, 2019