Vijana zaidi ya 1000 kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali vya ndani na nje ya nchi watakutanishwa jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Kimataifa utakaofanyika tarehe 24 Machi 2017 katika ukumbi wa Kardinali Rugambwa, Osterbay Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mwanzilishi wa Chama cha Kuweka na Kukopa cha Wajasiriamali Wanawake Tanzania (TASWE) Anna Matinde, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo leo jijini Dar es Salaam.
Matinde amesema kuwa TASWE kwa kushirikiana na Kikundi cha Kwaya ya Remnant Generation wameandaa Mkutano maalum kwa ajili ya vijana wa Vyuo Vikuu kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwabadilisha fikra ili watambue fursa zilizopo katika Sekta binafsi.
“Tarehe 24 mwezi Machi kutakuwa na Mkutano mkubwa wa Kimataifa ambapo vijana kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali watashiriki na kujengewa uwezo”. Amesema Matinde.
Kwa upande wake Katibu wa Vijana Wajasiriamali kutoka TASWE amesema kuwa lengo kubwa la mkutano huo ni kuwakutanisha vijana na kuwapa elimu itakayo wabadilisha mitazamo yenye lengo la kuwafanya wafikirie kujikita katika Sekta binafsi badala ya kutegemea kuajiriwa pindi watakapomaliza masomo yao ya elimu za juu.
Amesema kuwa sambamba na kubadilisha mitazamo yao mkutano huo utasaidia kuwaondolea msongo wa mawazo utokanao na ukosefu wa ajira pamoja na ukweli kwamba wahitimu wamekuwa wakiongezeka siku hadi siku huku ajira zikikua kwa kasi ndogo.
Mkutano huo wa Kimataifa wa Vijana unaandaliwa kwa ushirikiano baina ya Chama cha Kuweka na Kukopa cha Wajasiriamali Wanawake Tanzania (TASWE) na Kikundi cha Wanakwaya cha Remnant Generation kinachojali wahitaji kwa kusaidia mahitaji, ambapo Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Badilisha Mtazamo wa Vijana wajielekeze katika Sekta Binafsi”