Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema jumla ya vijiji 53 vya mkoa wa Njombe vitapatiwa huduma ya maji safi na salama katika mwaka huu wa fedha.
Majaliwa amesema hayo Januari 21, 201 wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Wanging’ombe katika mkutano wa hadhara katika kata ya Ilembula.
Amesema zaidi ya sh. bilioni 2.4 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia mradi huo wa maji katika miji ya Makambako, Njombe na wilaya ya Wanging’ombe.
Majaliwa amesema kuwa kati ya vijiji hivyo vitakavyopatiwa maji, vijiji 22 ni vya wilaya ya Wanging’ombe, hivyo aliwaomba wananchi hao kuwa na subira.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu tayari zabuni ya mradi huo imeshatangazwa, hivyo amewaagiza viongozi wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji watafute mkandarasi mzuri.
Amesema lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya maji katika umbali usiozidi mita 400 kutoka mahali anapoishi.
Aidha, Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Ally Kasinge kukutana na viongozi wa kata na vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Mapanga Kipengele ili kutatua kero ya mpaka.