Zoezi la Bomoa bomoa linaloendeshwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa lengo la kuondoa nyumba zilizojengwa katika maeneo ya wazi limeacha vilio na malalamiko kwa walioguswa.

Jana, Bomoa bomoa iliwakumba wakazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo takribani majengo ya makazi na maduka 15 eneo la Mwenge yalibomolewa.

Waathirika wa zoezi hilo walilalamikia utaratibu uliotumika wakidai kuwa hawakupewa taarifa mapema ili kuondoa mali zao. Baadhi ya wakazi hao walidai kuwa nyumba zao zilibomolewa huku mali zao zikiwa ndani, hivyo wamepata hasara kubwa ya kuanza upya maisha.

Katika hatua nyingine, Mkazi mmoja wa eneo hilo alisema kuwa zoezi hilo liliendeshwa kinyume cha sheria kwani bado kesi yao ya malalamiko iko mahakamani ikisubiri maamuzi ya mahakama.

Hata hivyo, Kamishna wa Ardhi wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusirika alisema kuwa kesi zilizoko mahakamani hazina uhusiano na zoezi wanaloliendesha na kwamba zoezi hilo liko kisheria kwani walishawaeleza watu wote waliovamia makazi ya wazi kuondoka mara moja.

Kamishina huyo aliwataka wananchi wote waliojenga katika maeneo ya wazi nchi nzima kubomoa nyumba zao wenyewe kabla hawajabomolewa na wizara hiyo na kwamba wanaweza kudaiwa gharama za kubomoa.

Baadhi ya wananchi waliokumbwa na zoezi hilo wilaya ya Kinondoni walidai hawana namna nyingi ya kuishi.

“Leo naona dalili za kulala nje na familia yangu kwa sababu sina sehemu ya kwenda. Kibaya zaidi sijaweza kuokoa kitu chochote, vyote vimeharibiwa,” alisema Atupokile Mwakasile, mkazi wa Kinondoni.

Vanessa Mdee arekodi wimbo na hitmaker wa ‘Duro’ Tekno wa Nigeria
Dk Tulia azungumzia taarifa zinazodai amepandikizwa Unaibu Spika