Viongozi wa vijiji vitano mkoani Morogoro wamejikuta matatani baada ya vijiji vyao kukutwa na mashamba ya bangi hekari 100 na kutakiwa kujisaimisha polisi.
Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa alitangaza kuwapa siku mbili viongozi hao kutoka vijiji vya
Bunduki, Misengere, Kododo, Vinile, na Yowe, Kata ya Doma wilayani Mvomero, vinavyozunguka Bonde la Mto Mgeta.
Amesema viongozi wa kijiji wanatakiwa kusema walikuwa wapi muda wote wakati shughuli hizo zikiendelea. Huku akiomba mamlaka za bonde zishirikiane na polisi kukabili kilimo cha bangi.
“Pia niombe mamlaka za bonde, TFS na mazingira ziangalie namna ya kushirikiana na jeshi la polisi na kuandaa operesheni ya pamoja na kuandaa oparesheni ya pamoja kwa lengo la kuondoa watu wote wanaofanya shughuli za kilimo katika misitu na kando ya mto Mgeta na hii itasaidia kudhibiti kilimo haramu cha bangi” Amesisitiza kamanda Mutafungwa.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Doma, Mapambano Mkopi, aliyeshiriki katika operesheni hiyo, alisema walishindwa kutambua uwapo wa shughuli hizo kutokana na umbali toka yalipo makazi ya watu.
Katika operesheni hiyo inayoendelea, watu 12 wanashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya.