Ili kuongeza kasi ya kuchanja chanjo dhidi ya Uviko-19 mkoani Rukwa, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti amezindua kampeni ya chanjo kwa Wahudumu wa afya ngazi ya Jamii, watu mashuhuri na viongozi wa dini.
Mkirikiti amezindua kampeni hiyo Sumbawanga Mkoani Rukwa, na kuwataka wataalamu wa afya kutoa ushirikiano wa karibu kwa wahudumu wa afya ngazi ya Jamii, watu mashuhuri na viongozi wa dini ili kuleta ufanisi katika utekelezaji wa afua ya uchanjaji chanjo ya Uviko-19.
Amesema, uzinduzi kwa ngazi ya mikoa umefanyika huku chanjo ikitolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya, na asilimia 10.1 ya wana Rukwa tayari wamechanja ikiwa ni idadi ndogo ikilinganishwa na mikoa mingine ya pembezoni kama Ruvuma 46% na Katavi 33%.
“Hii siku ya leo tunafanya uzinduzi kwa kutumia wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kuhamasisha ongezeko la watu wa mkoa huu kupata chanjo ya Uviko-19”, amesema Mkirikiti
Aidha, ameongeza kuwa uzoefu uliopatikana katika awamu hii na mikakati ya utekelezaji wa kampeni umeonyesha kuwa kasi ya matumizi ya chanjo dhidi ya Uviko-19 imeongezeka zaidi wakati wa kampeni na mwenendo wa hali ya uchanjanji ulishuka baadaye na kupelekea kutofikia malengo.
Hata hivyo, ametoa rai kwa wadau kushirikiana na timu za uendeshaji wa Huduma za Afya ngazi ya Mkoa na Halmashauri, ili kuhakikisha afua ya uelimishaji wa kutambua umuhimu wa chanjo, namna inavyofanya kazi na faida zake.
Mkirikiti ameongeza kuwa, zoezi hilo litafanikiwa kwa kuwapa elimu wananchi na kuwapatia chanjo kwenye matukio mbalimbali kama matamasha, michezo, magulio na sherehe za aina zote.
“Hakikisheni kuwa taarifa za wateja waliopata na wanaopata chanjo zinaingizwa katika mfumo wa chanjo kwa wakati na ufanisi mzuri na pia tuwape elimu wananchi na kuwapatia chanjo kwenye matukio mbalimbali,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa amemkumbusha waganga wakuu wa mikoa na Halmashauri nchini, kuhakikisha washirikishwa kikamilifu wakati wa utekelezaji wa afua za kuongeza kasi ya matumizi ya chanjo dhidi ya Uviko-19 wakati wote baada ya uzinduzi huo.