Scolastica Msewa – Kibaha.

Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ametoa muda wa siku 14 kukamatwa viongozi 24 wakiwemo Mabalozi, Wenyeviti wa Mitaa, Watendaji walioshirikiana na Madalali waliohusika kuwauzia Wananchi Viwanja katika eneo la shamba namba 34 la Mitamba mali ya Wizara ya mifugo na uvuvi.

Kunenge ametoa maagizo hayo hii leo Oktoba 13, 2023 wakati wa mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Pangani uliowahusisha watalaam kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha na mkoa kwa ajili ya kutoa msimamo wa serikali kuhusu maamuzi ya eneo hilo ambalo limevamiwa na wananchi kwa ajili ya makazi.

Amesema, anayo orodha ya majina ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia kinyemela wananchi viwanja katika eneo hilo ambalo linamilikiwa na serikali na kwamba anayakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Takukuru pamoja na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

Aidha Kunenge pia ametoa muda wa siku 60 wa Halmashauri ya Mji Kibaha, kupima eneo la shamba 34 la Mitamba lenye ukubwa wa hekta 4000 na kubainisha mipaka yote na matumizi yake ili ijulikane kama vile eneo la ujenzi wa ofisi za umma na huduma za kijamii, makazi kabla ya kuanza oparesheni ya kuwaondoa wananchi walio ndani ya shamba hilo.

“Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani pamoja na Takukuru ninayo majina 24 ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia wananchi eneo hilo la shamba namba 34 kinyemela, wahojiwe na sheria ichukue mkondo wake,” amesema Kunenge.

Amewataka pia Wananchi wote waliouziwa viwanja katika eneo hilo kufungua kesi dhidi ya waliowauzia na kwamba Serikali itatoa ushirikiano ikiwemo kuwatafutia Mawakili wa kuwatetea.

Amefafanua kuwa, majina ya waliyolipwa fidia kwa Wananchi kupisha eneo hilo yapo ambapo walilipwa fidia na kuainishwa kuwa eneo la hekta 2963 zirejeshwa kwa halmashauri kwa ajili ya kutumika kwenye shughuli za maendeleo na kubakiwa na eneo la hekta 1,037 ambazo hadi sasa zimebaki kwa ajili ya kutolewa maamuzi.

“Wananchi mjiandae tunasubiri maamuzi ya kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha kuridhia kuhusu matumizi ya eneo hili na baada ya watalaam kumege na kuyainisha maeneo kwa ajili ya shughuli za umma, taasisi mtapaswa kuondoka lakini litakalotengwa kwa ajili ya makazi basi mtauziwa, nawaomba kwa hiyari yenu muanze kuvunja nyumba zenu.

Akizungumzia historia ya eneo hilo, Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu, amesema kiwanja hicho kilipimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na kwamba mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo na kusema jitihada za kuwakataza wazanchi hao ziliendelea huku baadhi wakionekana kuendelea na shughuli za ujenzi walikaidi.

Amesema walipokea mapendekezo kutoa Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhusu upimaji wa eneo hilo ambapo hekta 150 zilitolewa kwa ajili ya Matumizi ya Wakala wa Maabara ya Vetenari Tanzania TVLA, hekta 188 kwa ajili ya matumizi ya Taasisi za Umma, 486 uwekezaji wa viwanda na 200 makazi.

Kuhusu uamuzi huo, Mwenyekiti Mtaa wa Lumumba mahali lilipo shamba hilo, Gideon Tairo amewaomba Wananchi kutoa ushirikiano pindi wataalam watakapofika kupima eneo hilo wasiwafanyie vurugu zozote na kumshukuru Mkuu wa Mkoa, Abubakar Kunenge kwa busara aliyoitumia kuwaelewesha wananchi kuhusu eneo hilo na kwamba wapo tayari kufuata utaratibu utaowekwa.

Martial ngoma ngumu Manchester United
Mohamed Makaka yu njiani Mtibwa Sugar