Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri na kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo wamefanya ziara na kutembelea vivuko vya feri na kubaini mapungufu matatu yanayokabili vivuko hivyo.
Ametaja mapungufu hayo kuwa ni kutokuwa na namba za dharura ndani ya kivuko na eneo la kusubiri kivuko, kutofanya kazi kwa runinga zilizopo kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya matumizi ya vivuko na kutokuwa na kamera maalumu za kurekodi matukio ya kinachoendelea ndani ya chombo hicho.
Hivyo ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa) kuhakikisha wanatatua changamoto hizo haraka iwezekanvyo na kudai kuwa endapo watashindwa kuboresha usafiri huo wa maji, vyombo hivyo vitasitishwa kuendelea kutoa huduma na wananchi watapaswa kutumia daraja la Mwalimu Nyerere.
“Tumebaini mapungufu mengi sana, nimetoa maelekezo kama hayatafanyiwa kazi tutafunga kwa sababu tuna daraja letu la Mwalimu Nyerere tutalitumia, Wakala wa Ufundi na Umeme msikariri kila kitu badilikeni na usafiri huu ni tofauti wananchi watapiga kwa namba gani kwa ajili ya msaada na hamna elimu ya uokozi” amesema Msafiri.
Aidha, Sara amesema ratiba ya ziara hiyo ilikwepo kabla hata ajali ya MV Nyerere haijatokea kwani ziara hiyo ilianzia nchi kavu na kumalizikia majini.
Kaimu mtendaji Mkuu wa Temesa, Mhandisi Sylivester Simfukwa amesema kazi yao kubwa ni kuhakikisha utekelezaji wa mambo yote yaliyoibuka na kuhakikisha usalama wa abiria wa kivuko cha majini na nchi kavu kwani suala la usalama wa abiria ni jambo ambalo linapewa kipaumbele sana.