Mashirika ya kutetea Wanahabari Sudan Kusini, yamezitaka mamlaka nchini humo kuwaachia huru waandishi 6 waliokamatwa kwa tuhuma za kusambaza video iliyomuonesha Rais Salva Kiir (71), akijikojolea.
Waandishi hao, wamezuiliwa kutokana na kusambaa kwa picha zinazomuonyesha Rais Kiir akitokwa na haja ndogo mwezi Desemba 2022 akiwa amesimama kwa ajili ya wimbo wa taifa katika hafla ya ufunguzi wa barabara.
Rais wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Sudan Kusini, Patrick Oyet amesema Waandishi hao wanaofanya kazi na Shirika la Utangazaji la Sudan Kusini linalomilikiwa na Serikali, walizuiliwa wiki iliyopita.
Waziri wa Habari wa Sudan Kusini, Michael Makuei na msemaji wa Idara ya Usalama wa Kitaifa, David Kumuri bado hawajatoa maoni yao kutokana na tukio hilo huku Maafisa wa Serikali wakikanusha mara kwa mara uvumi unaoenezwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Rais Kiir hayuko sawa.