Wabunge wa vyama vya upinzani vinavyounda Ukawa wamemuandikia barua Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Job Ndugai kuhoji uhalali na utaratibu utakaotumika wakati rais John Magufuli atakapolihutubia Bunge.

Wabunge hao wa Ukawa wamefanya mkutano na waandishi wa habari mjini Dodoma na kueleza msimamo wao kuwa watafanya maamuzi magumu ambayo hata hivyo hawakuyataja, endapo Rais John Magufuli ataongozana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein atakapoingia katika Bunge hilo kulihutubia kwa mara ya kwanza.

Akiongea kwa niaba ya wabunge hao wa Ukawa, mwenyekiti mwenza wa Umoja huo, Freeman Mbowe ameeleza kuwa tayari wamewasilisha barua yao  kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai kumueleza msimamo wao na kuhoji uhalali wa kikatiba wa Dkt. Shein kuhudhuria hotuba ya Bunge hilo.

Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu aliwataka wabunge kutoliacha suala la mgogoro wa Zanzibar katika mikono ya wazanzibar pekee kwa kuwa Tanzania ni moja.

“Sisi tunaofikiria kuwa haya ni mambo ya Wazanzibar tuwaachie na katiba yao, hatuponi kwa mujibu wa katiba hii,” alisema Tundu Lissu.

“Na kila mbunge tangu jana ameshika Biblia au Quran Tukufu na kusema kwamba atailinda, ataiheshimu na kuitii Katiba hii. Halafu tunaruhusu kiapo chetu cha Quran na Biblia Tukufu tunakikanyaga wenyewe kwa kunyamazia huu uchafu,” aliongeza.

Kumekuwa na mgogoro wa kikatiba kufuatia uamuzi wa Mwenyekiti wa ZEC, Jecha Salum Jecha kutangaza kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kwamba uchaguzi huo utarudiwa tena.

Uamuzi huo umepingwa vikali na CUF na Ukawa kwa ujumla huku ukiungwa mkono na CCM. Hata hivyo, tayari tangazo rasmi la kuufuta uchaguzi huo limeshachapishwa kwenye gazeti la Serikali ‘Gazette’.

Magufuli amteua Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu
Rufaa Za Vigogo Wa FIFA, UEFA Zakwama