Wabunge wanawake wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wametangaza rasmi ujiondoa katika Chama cha Umoja wa Wanawake (TWPG) , kupinga kitendo cha Mbunge la Ulanga, Godluck Mlinga (CCM) kudai kuwa wamepata ubunge kwa kufanya mapenzi, na kwamba  Mbunge huyo hajachukua hatua stahiki kuifuta kauli yake.

Akichangia katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria ya Mwaka wa Fedha 2016/17, Mlinga alisema kuwa wabunge wanawake wa Chadema hupata ubunge kwa kuitwa ‘baby’ na kwamba baadhi yao wanajihusisha na mapenzi ya jinsia moja.

“Kila mwanamke ndani ya chadema kaingia ubunge kwa sifa yake lakini sifa kubwa ni lazima uwe baby (mpenzi) wa mtu. Ndani ya Chadema kuna wapenzi wa jinsia moja,” alisema Mlinga.

Kupitia barua yao iliyosainiwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee kwa niaba ya wabunge wenzake wanawake, wabunge hao wamelaani kitendo cha Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson kuwataka wakae chini walipoomba miongozo wakitaka Mbunge huyo afute kauli yake.

Walieleza kuwa hawakuridhishwa na hatua ya Naibu Spika kuamua kuwa kauli hiyo ifutwe kwenye kumbukumbu za Bunge na kwamba alipuuzia madai yao ya kutaka Mbunge huyo kuwaomba radhi.

Aidha, wamewarushia lawama wabunge wenzao wanawake wa CCM kwa kile walichodai kutokemea na badala yake kushangilia wakati kauli hizo zinaondoa heshima na utu wa mwanamke. Wamesema wabunge hao wa CCM waliongozwa na aliyekuwa Katibu wa TWPG, Angela Kairuki na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge,Vijana, Ulemavu na Ajira, Jenista Mhagama.

“Ukimya wenu kwenye matukio haya na ushiriki wenu katika kushangilia wakati wanawake wanadhalilishwa inatufanya tuhoji mantiki ya uwepo wetu katika umoja huu ambao tunaambiwa malengo na dhamira yake ni kutuunganisha wanawake katika kumkomboa, kumpigania na kulinda haki na utu wa mwanamke,” inaeleza sehemu ya barua hiyo.

Hata hivyo, hivi karibuni, Mwenyekiti wa TWPG, Mama Magreth Sitta alilaani Bungeni kauli zote zinazolenga kudhalilisha wanawake na kueleza kuwa sio tu kwamba vinawadhalilisha wanawake bali vinaondoa heshima ya Bunge.

Polisi wa kike atumbuliwa jipu baada ya kupost ‘Selfie’ kwenye mtandaoni
Wimbo Mpya: Ali Kiba ft. M.I - AJE