Wabunge nchini Senegal wameingia katika sakata la kurushiana makonde na viti siku huku mmoja wao akimpiga kofi Mbunge wa kike usoni kutokana na mjadala wenye ukinzani kushamiri wakati wa kikao cha majadiliano Bungeni.
Hata hivyo, tukio hili linatokea wakati wa upigaji kura wa bajeti ya Wizara ya sheria ya mwaka ujao (2023), ukifanyika na uwasilishwaji wa bajeti ukiendelea huku Mbunge wa upinzani, Massata Samb alimpiga Amy Ndiaye Gniby wa muungano tawala wa Benno Bokk Yakaar (BBY).
Gniby alilipiza kwa kurusha kiti upande wa Samb kabla ya mbunge mwingine kumvuta hadi sakafuni na kupelekea kikao hicho kusitishwa lakini hata hivyo wabunge hao waliendelea kurushiana makonde na matusi.
Mzozo huo, ulitokea huku kukiwa na uhasama kati ya wanasiasa wa chama tawala na cha upinzani huku Wanaharakati wa wanawake na wanachama wa muungano unaotawala wakionesha kukerwa na shambulio la kimwili dhidi ya Ndiaye.
Wanaharakati hao, wamesema wataendesha kampeni ya uhamasishaji kuhusu unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kwakua tukio hilo limechukua taswira mpya na kusambaa kote ulimwenguni kitu ambacho kinaweza kuleta athari na mkanganyiko.
Mvutano kati ya wanasiasa watawala na wa upinzani umekuwa ukiongezeka ambapo uchaguzi wa wabunge wa Julai, 2022 ulishuhudia chama tawala kikipoteza wingi wake wa kura kutokana na uwepo wa hofu kwamba Rais Macky Sall atawania muhula wa tatu mwaka wa 2024.