Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, limefanikiwa kukamata jumla ya Mifugo 400 ambayo ilikua inasafirishwa kwenda Nje ya Nchi bila kufuata utaratibu.
Akitoa taarifa hiyo hii leo Oktoba 28, 2023, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Simon Pasua amesema Mifugo hiyo imekamatwa katika Wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga, kupitia doria ambayo bado inaendelea.
Amesema, katika kuhakikisha wafugaji na wafanyabiashara wanafuata taratibu, kwa mwezi Oktoba mwaka huu Jeshi hilo limefanikiwa kutoa elimu kwa wafugaji katika minada mbalimbali nchini ambapo hadi kufikia Oktoba 28 jumla ya vipindi 149 vya elimu vimetolewa kote nchini.
ACP Pasua amefafanua kuwa, kupitia elimu ambayo wanaendelea kuitoa imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya wizi wa mifugo sambamba na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Aidha, ametoa wito kwa wafugaji wote nchini kuacha mara moja tabia ya kuhamisha mifugo kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine ama Nchi jirani bila ya kufuata utaratibu wa kupata vibali toka serikalini, kwani Jeshi hilo litachukua hatua za kisheria dhidi yao ikiwa ni pamoja na kukamata mifugo hiyo na kuwafikisha mahakamani.
Kwa upande wake Msimamizi wa Mnada wa Horohoro uliopo Mkoani Tanga, Edgar Ndombere pamoja na kulishukuru Jeshi hilo kwa doria ambayo wanaendelea kuifanya, amesema changamoto wanayokutana nayo ni wafugaji wengi kutokua na utayari wa kulipa kodi ambapo hupita sehemu ambazo sio rasmi.
Aidha ametoa wito kwa wafugaji hao kuwa wazalendo na kufuata utaratibu uliowekwa kwa kuhakikisha wanapeleka mifugo yao katika maeneo ya minada ili wapatiwe vibali kwa ajili ya kusafirisha mifugo yao.