Wadau wa Asasi za kiraia na za Serikali wamesema ipo haja ya ushirikishwaji wa kikamilifu kwa waandishi wa habari kushiriki michakato ya uundwaji au urekebishwaji wa sheria mbalimbali zinazohusu tasnia ya Habari nchini.
Hayo yamebainishwa na wadau hao wakati walipokutana Wilaya ya kati mkoa wa kusini Unguja, kuzungumzia na wadau kutoka taasisi mbali mbali za Serikali na zisizo za kiserikali katika mkutano wa siku moja uliolenga la kuzipitia na kutoa maoni ya baadhi ya sheria ikiwemo sheria ya Tume ya Uchaguzi, habari na sheria ya Takwimu Zanzibar.
Wamesema ‘’Ili kuepuka haya ni vyema sisi waandishi wa habari tukashirikishwa kikamilifu tangu hatua za awali kwenye uundwaji wa sheria ili kutoa maoni yetu pale tunapoona hapatakua sawa hususani katika utendaji wetu wa kazi.’’
Awali, mwanahabari mwandamizi Zanzibar Salim Said Salim alisema kuna baadhi ya sheria ni za ajabu sana, alitolea mfano kipengele cha sheria ya Uchaguzi kinachomkataza mwandishi wa habari kutojumuisha matokeo ya uchaguzi yaliobandikwa ukutani katika vituo vya kupigia kura, matokeo ambayo tayari yamewekwa kwa ajili ya umma na maafisa wenyewe wa tume hiyo.
Amesema, ‘’Kwa kuwa maafisa wenyewe wa tume ya uchaguzi ndio waliojumlisha na kubandika matokeo ya kura kwenye vituo vya kupigia kura huku karatasi hizo zikiwa tayari zimetiwa saini za wahusika kwanini mwaandishi wa habari azuiwe keshiria kufanya kazi yake ya kutoa taarifa hizo za idadi ya kura husika kutoka kwenye vituo.’’
Naye mratibu wa Baraza la Habari Tanzania MCT, Shifaa Said Hassan alisema kuwepo kwa sheria bora katika nchi zitasaidia kuleta usawa na demokrasia, sambamba na hilo alisisitiza umuhimu wa kufuata na kutekeleza kwa vitendo mikataba ya Kikanda na Kimataifa ambayo nchi imeridhia ni jambo la msingi na linalopaswa kutiliwa mkazo zaidi.