Wadau wa Haki ya Kupata Habari nchini (CoRI), wamefanya mazungumzo na baadhi ya wabunge, wakilenga kuongeza ufahamu kuhusu mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari nchini ambayo imekuwa ikipigiwa kelele na watu wengi hasa wanatasnia.
Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dodoma Novemba 10, 2022 yakiongozwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Vyombo ya Habari Kusini mwa Afrika, Tawi la Tanzania (MISA TAN), James Marenga na Balile waliwaonesha wabunge baadhi ya vipengele vya sheria ya habari ya mwaka 2016 na mapendekezo ya wadau wa habari.
Hata hivyo, Wabunge hao waliuliza maswali kadhaa yalitolewa ufafanuzi toka kwa Balile na Marenga na pia walieleza kufurahishwa na umoja wa wadau wa habari, ulioundwa kwa ajili ya kufanikisha mapendekezo ya mabadiliko ya sheria ya habari.
Wabunge hao, wameahidi kufanyika kazi suala hilo na hatimaye kuwa na uelewa ili suala hilo litakapofikishwa mbele yao, wapate kuishauri Serikali kwa malengo mapana ya taifa.