Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla amewashukuru Wafanyabiashara wa Kariakoo kwa kuamua kuhama ili kupisha uchunguzi na ukarabati na kuahidi kuratibu zoezi la kuhama na kutunza orodha yao ili watakapokwenda Kisutu na Machinga Complex wasilipe Kodi kwa miezi miwili.
RC Makalla amesema hayo alipokuwa akizungumza na Wafanyabiashara hao ambapo amewataka kuhakikisha kabla hawajaondoka wahakikishe wameratibiwa taarifa zao.
Aidha RC Makalla amesema Serikali ya Mkoa imejipanga kuhakikisha hakuna mfanyabiashara atakaekosa eneo la kufanyia Biashara.
Kuhusu Wafanyabiashara Soko dogo, RC Makalla amesema biashara ziendelee lakini tayari ametuma timu ya wataalamu wa Ujenzi kwajili ya kufanya tathimini endapo Soko kubwa litakarabatiwa na kukaonekana umuhimu nalo lifanyiwe ukarabati hapo baadae.
Pamoja na hayo RC Makalla amesema kwa wakati huu Wafanyabiashara Soko dogo wataendelea na biashara zao Kama kawaida huku akisisitiza agizo la kutaka Barabara za kuingia sokoni hapo kuachwa wazi.