Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amewataka wakazi wa mkoa huo kuchangamkia fursa za kibiashara kutokana na ujio wa Kongamano la Kimataifa la Utalii, litakalofanyika katika viwanja vya Kihesa Kilolo.
Dendego ameyasema hayo, wakati akizungumza na waandishi wa habari na kuongeza kuwa ujuo wa Kongamano hilo ni nafasi adhimu kwa wakazi wa Mkoa wa Iringa, hivyo ni muhimu wakajiandaa kulipokea na kuchangamkia fursa za kiutalii.
Amesema, kongamano hilo linalotarajiwa kuanza mwezi Novemba 9 hadi Novemba 13, 2022 na limelenga kufungua milango ya utalii Kusini mwa Tanzania ikiwemo kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana katika mikoa 10 ya ukanda huo.
Aidha, ameitaja Mikoa inayotarajia kushiriki kongamano hilo kuwa ni Iringa, Mbeya, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, Lindi, Njombe, Songwe na Morogoro na kusema “Hili ni kongamano lenye hadhi ya Kimataifa kwa hiyo changamkieni huu fursa, uwe mfanyabiashara mdogo au mkubwa nafasi ipo.”
Awali, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Mkoa wa Iringa, Jimson Sanga alisema kongamano hilo litasaidia kukuza sekta ya utalii kwenye mikoa hiyo na kuongeza ari ya wageni kutembelea vivutio vya kitalii vinavyo patikana katika mikoa hiyo.