Mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli ambaye pia ni Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaahidi wakazi wa Kakonko kuwa iwapo watamchagua kuwa rais kwa awamu ya pili, atawapa majengo ya kambi za wakandarasi zilizopo katika eneo hilo.
Dkt. Magufuli ametoa ahadi hiyo wakati akinadi sera zake kwa wakazi wa Kakonko mkoani Kigoma, akisema kuwa atawapa bure wakazi hao majengo hayo ili waweze kupanga wayatumie vipi iwapo watatumia kama hospitali, shule ama matumizi mengine yatakayowanufaisha.
Dkt. Magufuli ameeleza kuvutiwa na uzuri wa majengo hayo ambayo yanatumika na wakandarasi wanaoendelea na ujenzi wa barabara na kusema kuwa punde baada ya kukamilikka kwa mradi huo atawakabidhi wakazi wa Kakonko mradi huo iwapo atakuwa rais.
“Lakini mnafahamu, kuna makandarasi ambao wana kambi yao pale chini, nilikuwa naiona ile kambi ni nzuri sana, watakapomaliza kutengeneza barabara, mtapanga nyinyi hapa Kakonko mnataka myatumieje, nitawapa bure,”amesema Magufuli.
Aidha, amesema kuwa serikali inaendelea na ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Kakonko ambayo endapo chama hicho kitafanikiwa kurudi madarakani, hospitali hiyo itamaliziwa, na serikali yake inatarajia kuiwezesha hospitali hiyo kuweza kutoa huduma za upasuaji.
Mgombea huyo anatarajiwa kuendelea na mikutano yake ya kampeni mkoani Kigoma leo Septemba 17, 2020.