Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), wamesisitiza umuhimu wa soko la pamoja katika kukuza uchumi wakati waliposhiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mkutano huo, maalum wa ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Arusha ni sehemu ya mikutano ya awali kuelekea Mkutano wa 22 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika tarehe 22 Julai 2022.
Wakuu wa Nchi wamejadili na kuyawekea msisitizo masuala mbalimbali ya hali ya halisi ya utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja la Jumuiya ya Afrika Mashariki
sambamba na kuainisha changamoto zinazohitaji ufumbuzi wa pamoja katika kuyafikia malengo ya jumuiya hiyo.
Akichangia mada wakati wa mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwenyeji wa mkutano huo, amesisitiza juu ya kukuza uzalishaji pamoja na kuongeza thamani ya mazao na bidhaa zinazozalishwa ndani ya jumuiya ili kuweza kuingia katika ushindani wa kibiashara kimataifa.
Aidha, amefafanua kuwa katika kuyafikia malengo ya pamoja ni muhimu kwa nchi wanachama kuwekeza katika amani na utawala bora ili nchi ziweze kuongeza nguvu katika usimamizi wa rasilimali na uzalishaji badala ya kuwekeza katika migogoro.
Naye, Mwenyekiti wa mkutano huo na Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta amesisitiza umuhimu wa kuwa na mawasiliano kupitia ujenzi wa miundombinu ambao ndio msingi mkuu wa kuyafikia malengo ya soko la pamoja.
Amesema kwa sasa nchi wanachama zimeunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu ya kisasa na akatolea mfano ujenzi wa reli ya kisasa unaofanywa na Tanzania ambao utaziunganisha nchi wanachama na kwamba kwa upande mwingine Tanzania na Kenya zinaunganishwa kupitia ujenzi wa miundombinu uliofanywa mipakani katika eneo la Namanga na Taveta.
Maeneo mengine yaliyojadiliwa ni nchi zilizoongezeka kufuatia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kujiunga na jumuiya hiyo, umuhimu wa usimamizi wa rasilimali kama vile
madini na umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi katika kuyafikia malengo yaliyowekwa.
Hata hivyo, wakuu pia walijadili mafanikio yaliyofikiwa na jumuiya hiyo ikiwemo, uhuru wa kufanya biashara, mtangamano wa kijamii na fursa za kuvuka mipaka kupitia Hati ya
kusafiria ya kielektroni ya Afrika Mashariki na kuondoleana visa miongozi mwa nchi wanachama.
Mkutano huo umehudhuriwa na Nchi zote saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni pamoja mwenyekiti wa mkutano huo Jamhuri ya Kenya, Mwenyeji wa mkutano Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Rwanda, Jamhuri ya Sudan Kusini, na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo na mgeni mwalikwa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia.