Tanzania inatarajia kuwa kitovu cha biashara ya madini kwa kuvutia wawekezaji wengi duniani kuja kuwekeza katika sekta hiyo na kufungua fursa nyingi za kuchimba madini.

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko ameyasema hayo Mkoani Kigoma, wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini katika mkutano uliolenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu shughuli za uchimbaji.

Amesema, mataifa mengi yanakuja nchini kujifunza kuhusu usimamizi wa Sekta ya Madini na hasa sekta ndogo ya wachimbaji wadogo na hivyo kuifanya Tanzania kuwa mfano kwa mataifa.

Waziri wa Madini, Doto Biteko

“Serikali imeendelea kutengeneza mazingira rafiki kwa wachimbaji katika Sekta ya Madini kuweza kuwekeza katika uchimbaji wa madini na kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara hiyo na Rais Samia anawapenda na kuwathamini sana, anatamani kuona changamoto mlizonazo zinamalizwa haraka,” amesema Waziri Biteko.

Kuhusu mikopo kwa wachimbaji wa madini, Biteko amesema Serikali imefanya kazi kubwa kuzungumza na taasisi za fedha ili zianze kukopesha wachimbaji wadogo na tayari zipo baadhi ya taasisi zinazotoa mikopo kwa wachimbaji.

Ameongeza kuwa, Sekta ya Madini ina wajibu wa kutoa ajira kwa Watanzania, kukuza uchumi wa nchi na kujenga utajiri na kuwaondolea umaskini watu na kwamba inatatua changamoto ya soko kuu la madini la mkoa kwa kuendelea na ujenzi wake ambao utasaidia uuzaji wa madini.

Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na wachimbaji wadogo wa Madini Mkoani Kigoma.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amewapongeza wachimbaji wa mkoa wa huo kwa kufanya kazi na kuendelea kuutangaza mkoa kwa uchimbaji madini katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wachimba Madini Mkoa wa Kigoma (KIGOREMA), Lister Balegele amesema lengo la chama hicho ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanakuwa na viwango vya kutoa tija katika soko la ndani na nje ya nchi na kudhibiti uchimbaji holela wa madini usiofutata Sheria na Taratibu zilizowekwa na Serikali.

Afisa Madini Mkazi wa Kigoma, Mhandisi Pius Lobe naye amesema, mkoa huo una jumla ya leseni 429 za uchimbaji mdogo wa madini, leseni mbili za uchimbaji wa kati wa madini. Nyingine ni leseni tisa za utafutati mkubwa wa madini, leseni nane za biashara ndogo ya madini na leseni 11za biashara kubwa ya madini.

Abdul Sopu afunguka alivyozikataa Simba SC, Young Africans
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Julai 21, 2022