Makada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), ‘Waliokatwa mikia’ wamekuwa wakizunguka katika ofisi ndogo za makao makuu ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam kwa lengo la kujionyesha na wakati mwingine kuomba kazi za kujitolea.

Jina la Makada ‘Waliokatwa mikia’ lilianzishwa na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Dkt. John Magufuli ambalo alilitoa julai 23 mwaka 2016 wakati wa mkutano mkuu wa kumkabidhi kijiti cha uenyekiti kutoka kwa mtangulizi wake, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.

Rais Magufuli alifananisha na Ng’ombe waliokatwa mikia kuwa wakirudi zizini ni rahisi kuonekana huku Ng’ombe wenzao wakiwashangaa.

Kauli hiyo ilikuwa ikimaanisha kuwa waliokatwa mikia ni wale ambao walikuwa CCM na baadaye wakaamua kuhamia upinzani, lakini baadaye waliomba kurudi tena CCM na wakakubaliwa.

Aidha, mwaka 2015 wakati wa kampeni za kuwania urais, baadhi ya makada wa CCM walisombwa na ‘Mafuriko’ ya aliyekuwa mgombea wa urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa akitokea CCM ambaye aliungwa mkono na Vyama Vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Baada ya ushindi wa Rais Magufuli baadhi ya wanachama waliofuata upepo wa Lowassa walirudi CCM wakitarajia neema ya kuteuliwa ama kwenye nafasi ya serikali au ndani ya chama, huku wengine wakitarajia neema katika biashara zao.

Hata hivyo, neema hiyo iliwaangukia wachache huku wengine wakijikuta hawakumbukwi kwenye nafasi yoyote na hawana thamani tena bila kujali nafasi walizokuwa nazo wakati wanaondoka, ambapo hali hiyo imesababisha wengine kuanza kulalamikia mazingira magumu waliyonayo kwasasa.

Nafasi walizotarajia kupata baada ya kurudi CCM ni pamoja na zile za kiserikali, Ukuu wa mkoa (RC), Ukuu wa wilaya, (DC), Katibu tawala mkoa (RAS),Katibu tawala wilaya (DAS) ambazo zingine zimechukuliwa na makada wapya kutoka upinzani.

 

Kiswahili Lugha Rasmi SADC!
LIVE DAR ES SALAAM: Ufungaji wa mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi za Kusini mwa Afrika SADC