Polisi nchini Hispania, wamewakamata wapenzi wawili waliokiri kuwa ni washirikina baada ya kukutwa makaburini usiku wa manane wakifanya shughuli za kichawi walizodai zinalenga kulinda penzi lao.
Katika tukio hilo, Polisi wa doria walishitushwa na mwanga wa mishumaa uliokuwa ukiangaza kwenye makauburi ya umma ya jijini Madrid, na waliposogea eneo hilo waliona wapenzi hao wamezungukwa na mifupa ya binadamu, vibuyu na nguo nyeupe huku wakifanya ishara za ajabu.
Mara baada ya kuhojiwa, watu hao walisema wapo mahala hapo kufanya kafara ya kuwasahau wapenzi wao wote wa zamani, ili wasisalitiane katika penzi lao jipya lililochipua hivi karibuni.
Hata hivyo, kwa uungwana Polisi waliwasubiri wapenzi hao kumaliza shughuli zao na kisha walichukua na kwenda nao kituoni, ili kuwahoji walipata wapi mabaki ya miili ya binadamu waliyokuwa wakiitumia katika tambiko.