Jeshi la Nigeria limetangaza kuwapata wanafunzi wawili wa zamani wa kundi la “Chibok girls”, waliotekwa nyara na kundi la wanajihadi la Boko Haram miaka minane iliyopita.
Wasichana hao, wamepatikana wakiwa tayari wana watoto kila mmoja na waliwasilishwa kwa vyombo vya habari na jeshi ili waweze kutambuliwa na familia zao.
Kamanda wa Kijeshi katika eneo hilo, Jenerali Christopher Musa amewaambia waandishi wa habari kuwa wasichana hao walipatikana Juni 12 na Juni 14, 2022 katika maeneo mawili tofauti.
“Tuna bahati sana kuwapata wasichana hawa wawili wa Chibok, na ni jambo jema kuwa wapo hai ingawa tayari ni wazazi kwani kila mmoja ana mtoto, lakini wanaweza kuungana tena na familia zao,” alisema Musa.
Wasichana hao wawili walikuwa ni miongoni mwa wanafunzi 276 wenye umri wa miaka 12 hadi 17 waliotekwa nyara kutoka shule yao ya bweni huko Chibok, kaskazini-mashariki mwa Nigeria.