Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekagua miradi miwili ikiwemo wa ujenzi wa kiwanda cha kusarifu dagaa, ZAFICO na kuwaagiza Jeshi la Kujenga Uchumi -JKU, ambao ni mkandarasi kuwalipa fidia Wananchi waliovunjiwa vibanda.
Dkt. Mwinyi ametoa maagizo hayo, wakati akizungumza na Wananchi katika eneo la mradi Wilaya Magharibi A Mkoa wa Mjini Magharibi, huku akiwapa JKU muda hadi Desemba 8, 2023 wawe wamekamilisha ujenzi wa mradi huo na kuahidi kutembelea tena kugagua maendeleo ya ujenzi.
“JKU iwalipwe fidia zao Wananchi na hili nitalifuatilia kuhakikisha watu hawa wanalipwa stahiki zao haraka, wakiwemo vibarua ambao awali walilalamika kucheleweshewa malipo yao,” amesema Dkt. Mwinyi.
Rais Dkt. Mwinyi pia alitembelea mradi wa Bandari kavu ya Maruhubi iliyopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, eneo ambalo linatumika kuhifadhi na kutoa makasha (makontena).