Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo, Othman Masoud Othman amewataka viongozi na wanachama kutovunjika moyo na badala yake waendelee kuwajibika ili kueleta ufanisi na kutimiza dhamira na malengo yao.
Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo katika ziara ya kuimarisha chama Jimbo la Mtoni wilaya ya Mgharib ‘A’ Unguja, wakati akizungumza na viongozi wa chama wa jimbo.
Amesema, ni muhimu kwa viongozi na wanachama kutokata tamaa na kuwataka wanachama na viongozi wote kwa umoja wao kuwakataa wale wote wanaojenga mfarakano katika chama kwa nia ya kujipanga katika kuwania nafasi za uongozi wa ngazi mbali mbali.
Aidha, amewataka kuendelea kujitolea na wasiwabeze wala kuwakataa watu wanaojiweka mbele kwani wanachangia mafanikio katika harakati za chama na kudai kuwa uhai wa chama ni cha wanachama si viongozi huku akihimizia wote kuchangia maendeleo ya chama.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Ismail Jussa Ladhu amewataka wanachama hasa vijana kuendeleza ari ya kukijenga chama, ili kuleta fikra za mabadiliko kupitia nchaguzi huru na haki.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binaadamu wa Chama hicho, Pavu abdalla Juma amesema kuna haja ya Serikali kuhakikisha zinashughulikiwa changamoto za barabara za ndani ya Jimbo hilo ambazo ni kero wakati wa dharura hasa ugonjwa.