Wanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Msumbiji wamedai kupakwa kinyesi, kulishwa na kunyweshwa mikojo katika sherehe za kukaribishwa katika chuo hicho.
Picha za tukio hilo zilizosambaa mitandaoni zimezua gumzo kwenye mitandao na kulaaniwa vikali. Wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza wanaeleza kuwa walifanyiwa ukatili huo na wanafunzi wa mwaka wa pili ambao ndio waliokuwa waandaaji wa sherehe hizo, katika mkoa wa Zambezi.
Waathirika wa tukio hilo wameeleza kuwa walijikuta katika wakati mgumu wakilazimishwa kunywa mikojo na kula kinyesi, tofauti na mapochopocho waliyokuwa wanaamini watayapata kama ilivyo kawaida kwa sherehe zozote, kwa mujibu wa kituo cha runinga cha STV nchini humo.
”Waandalizi wa sherehe hiyo walitukata nywele zetu .Ilikuwa inatisha, ilikuwa haiwezi kuvumilika.Walitulazimisha kunywa mikojo na kula kinyesi . Tuliogeshwa mikojo huku wakifuta pua zetu na vinyesi,” alieleza mwanafunzi aliyejitambulisha kwa jina la Artemiza Nhantumbo.
Kutokana na tukio hilo, wazazi pamoja na wadau wa elimu nchini humo wametaka wahusika wachukuliwe hatua kali pamoja na wasimamizi wa chuo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na STV, wanafunzi wa mwaka wa pili walioshiriki katika tukio hilo tayari wamefukuzwa chuo wakisubili hatua nyingine za kisheria dhidi yao.
Mkurugenzi wa elimu ya juu mkoani humo, Cardoso Miguel amesema kuwa ameunda kamati maalum ya kuchunguza tukio hilo huku akisisitiza kuwa kutokana na picha alizoziona kwenye mitandao ya kijamii, tabia iliyofanywa haifai.