Wanafunzi wa Darasa la Saba Shule za Msingi za Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu wamemuomba Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kuwataka wasimamizi wa Mtihani wa Taifa wenye tabia ya kuwatisha wanafunzi wakiwa katika chumba cha mtihani waache tabia hiyo ili wanafunzi wafanye Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba, mwaka 2018 kwa uhuru pasipo uoga.
Wametoa ombi hilo wakati Mkuu huyo wa Mkoa alipokutana na wanafunzi wa darasa la saba takribani 782 wa shule tano za msingi za Mjini Bariadi, katika Shule ya Msingi Sima B, lengo likiwa ni kuwahimiza kusoma kwa bidii katika siku chache zilizobakia na kuwatakiwa kila la heri katika mtihani wa Taifa utakaofanyika Septemba 05 na 06 mwaka huu.
Aidha, wamesema kuwa wamepata taarifa kutoka kwa wenzao waliowatangulia kuwa siku za nyuma kulikuwa na baadhi ya wasimamizi wa Mtihani wa Darasa la Saba ambao walikuwa wakiwatisha na kuwanyanyasa watahiniwa, hivyo kuwafanya wanafunzi kufanya mtihani wakiwa na hofu jambo lililofanya baadhi yao kushindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.
“Miaka ya nyuma tunasikia kuna wasimamizi walikuwa wanawatishia sana wanafunzi, tunaomba Mkuu wa mkoa utusaidie na sisi wasije wakatutishia tukashindwa kufanya mtihani wetu wa Taifa vizuri,” amesema John Isack Mwanafunzi wa darasa la Saba Shule ya Msingi Sima A, Bariadi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewahakikishia wanafunzi hao kuwa hakutakuwa na vitisho wala manyanyaso yoyote kutoka kwa wasimamizi wa mitihani na akawaeleza kuwa atakutana na wasimamizi wa mitihani ambao wapo katika semina elekezi na kuwapa angalizo hilo.
Akizungumza na wasimamizi wa Mtihani wa Darasa la Saba, Mtaka amewataka wasimamizi hao ambao ni walimu kuwasimamia wanafunzi hao huku wakitambua kuwa wao ni walezi, hivyo wanapaswa kusimamia kwa kufuata taratibu zilizowekwa pasipo kuwatisha wala kuwanyanyasa watahiniwa.
-
JPM ahoji ubaya wake upo wapi, awakumbusha haya wafanyakazi
-
Serikali yapanga kuzalisha Mitamba zaidi ya mil. 1 kwa mwaka
-
Video: Matukio ya ukatili kwa Wanawake na Watoto yameongezeka- LHRC
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kutoa zawadi ya shilingi milioni moja kwa mwanafunzi wa kiume, milioni moja na laki tano kwa mwanafunzi wa kike atakayekuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora Kitaifa katika Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Darasa la Saba mwaka 2018 na shilingi milioni tatu kwa Shule ya Msingi ya Mkoa huo itakayokuwa miongoni mwa shule kumi bora Kitaifa.